EMI SCHOOLS CENTRE, We Lead and let other follow.

EMI SCHOOLS CENTRE

We lead and let others follow!

MJI WA MUNGU VIKUGE.

A. UTANGULIZI:

MJI WA MUNGU VIKUGE ni Mji watakaokuwa wakiishi watoto YATIMA ambao wamefiwa na wazazi wao wakiwa bado wachanga/wadogo, lakini pia wapo wale watakaookotwa baada ya kutupwa na wazazi wao mara tu baada ya kuzaliwa na wazazi wao kutoweka. Mji huu pia utalea na kutunza watoto wa mitaani ambao wamekumbwa na tatizo/ changamoto ya wazazi kutengana katika maisha ya kifamilia na kuachwa bila uangalizi.
MJI HUU UPO KIBAHA MKOA WA PWANI KATA YA SOGA. WASTANI WA KILOMETA 3.5 TOKA BARABARA KUU YA MOROGORO BARABARA YA SOGA IENDAYO KITUO KIKUU CHA RELI YA MWENDO KASI SGR.
Kazi kubwa ya wasimamizi na watendaji katika Mji huu ni kuwapa makundi haya ya watoto huduma za kijamii ambazo wangezipata endapo wazazi wao wangekuwa hai. Hapa watapewa malezi bora kulingana na umri wao toka uchanga, utoto, ujana hadi kufikia umri wa kujitegemea.Huduma muhimu za kibinadamu kama chakula, mavazi, elimu,matibabu vitatolewa BURE kwa watoto watakaokuwa katika Mji huu.
Tunakaribisha jamii yote ituunge mkono ili kufanikisha jambo hili.
EMI SCHOOLS' tumekuwa tukitoa huduma hii toka mwaka 2013 katika mazingira ya kifamilia. Lakini imefika wakati sasa imetulazimu tulipanue ili kusudi Serikali na jamii kwa ujumla iwaone watoto hawa mahali walipo ili wapate msaada kwa upana na marefu zaidi. Ndio maana tukajenga MJI huu wa MUNGU VIKUGE ili waishi hapo waonekane vizuri na kwa uwazi zaidi.
Hadi kufikia Septemba 2025 Mwenyezi MUNGU ametusimamia hadi tukakamilisha kupata shamba tumejenga majengo ya kuanzia na sasa tunaanza MJI Rasmi wa YATIMA ambao utajitegemea katika kujiendesha kwa hali yeyote ile mbali na kupata misaada toka sehemu mbalimbali.

B. UONGOZI.

Mkurugenzi Mkuu mwanzilishi atateua wakurugenzi wasaidizi watakaomsaidia katika kuendesha MJI wa MUNGU VIKUGE. Miongoni mwa wakurugenzi watakaoteuliwa mmoja atakuwa ni
1. Katibu Mkuu ambaye kazi yake kubwa ni kupokea maelekezo toka kwa Mkurugenzi Mkuu na kuyatekeleza kila siku.
a) Pia atasimamia kazi za kituo chote kwa namna ratiba itakavyopangwa.
b) Atatunza kumbukumbu zote za kituo.
c) Ataongoza kituo wakati ambapo Mkurugenzi Mkuu hayupo au ameshindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na afya yake au umri wake.
d) Ataajiri watumishi wakaosaidia katika kazi ndogondogo za kila siku katika Centre kama vile ufugaji, kilimo, usafi nk.
e) Atashirikisha wakurugenzi wengine katika maamuzi makuu yanayohusu Centre kama vile Bajeti ndogo ya wiki, Matumizi ya dharura
yanayozidi Tsh Millioni moja na kusimamishwa kazi mtumishi yeyote.
Mkurugenzi msaidizi wa pili aliyebaki atafanya majukumu yafuatayo:-
a) Atashughulikia mambo yote yanayohusu elimu ya watoto Yatima watakao kuwa wanalelewa hapa katika MJI WA MUNGU VIKUGE kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu.
b) Atahakikisha kuwa watoto Yatima wanaomaliza elimu ya Msingi/Sekondari katika shule za EMI wanapata nafasi za masomo katika mashule mengine au Vyuo vya elimu ya Ufundi au elimu ya juu hapa nchini hata NJE YA NCHI kwa kushirikiana na Serikali.

C. USIMAMIZI WA CENTRE.

(i) Centre itasimamiwa na Mkurugenzi Mkuu mwanzilishi wa Taasisi ya EMI. Chini yake kutakuwapo na Wakurugenzi wasaidizi. Chini ya hawa wasaidizi watakuwa maafisa waandamizi ambao ni Afisa Ustawi wa Jamii, Mlezi wa Watoto (Matron) na wafanyakazi katika idara mbalimbali kulingana na uhitaji wa Centre ambao ni watumishi wa kulipwa.

USIMAMIZI WA MATUMIZI NA MAPATO YA CENTRE

a) MFUKO WA MJI WA MUNGU:-
Mkurugenzi mwanzilishi ataanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kupata pesa ya kuendeleza mfuko huu ambao utaendeshwa kwa misingi ya kuhudumia Yatima tu na si vinginevyo.
Ili kutunisha mfuko huu ni lazima kuwe na vyanzo vya uhakika vya mapato ili kusudi familia hii ya YATIMA isikose huduma wakati wote. Hivyo vyanzo vya mapato ya mfuko wa MJI WA MUNGU ni pamoja na:-
i. Uzalishaji wa fedha itakayotokana na miradi mbalimbali ya Centre.
ii. Michango/Misaada itokanayo na Mkurugenzi Mkuu mwenyewe.
iii. Misaada toka kwa wasamaria wema na wafadhili mbalimbali toka nje na ndani ya nchi pia.
iv. Mikopo yenye riba kidogo au isiyokuwa na riba kabisa na isiyo na masharti ya kuifilisi familia ya YATIMA.
b) Mapato yote yatakayokuwa yakikusanywa yatawekwa katika Akaunti ya Bank ambayo itakuwa ikiendeshwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi.
c) Matumizi ya Taasisi yatapangwa na Mkurugenzi Mkuu akishauriana na Wakurugenzi wasaidizi kulingana na mahitaji ya kila wakati.

D. KUMILIKI MALI.

i. MJI WA MUNGU VIKUGE utamiliki mali inayohamishika na isiyohamishika popote katika Jamhuri ya Muungano na hata nje ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ii. Mkurugenzi Mkuu mwanzilishi na atakayerithi kiti hicho atamiliki mali hizo kwa niaba ya MJI WA MUNGU VIKUGE (MMV)

E. MIRADI MUHIMU.

Miradi muhimu tunayotegemea kuanzisha ili kuwezesha kituo kujiendesha kwa mahitaji muhimu ya kibinadamu bila kuwa ombaomba ni kama ifuatavyo:-
i. KILIMO:
Tutazalisha mboga na matunda mbalimbali Matumizi: Tutakula na kuuza, Tutazalisha mahindi, kunde na mbaazi. Matumizi: Tutakula na tutauza.
ii.MIFUGO:
Tutafuga kuku, sungura na samaki
Matumizi: Tutakula na kuuza
Tutafuga ng'ombe wa maziwa
Matumizi: Tutakunywa maziwa na tutauza maziwa na ndama, tutapata mbolea kwa ajili ya kilimo.
iii. BIASHARA:
Tutajenga fremu za biashara eneo la mbele (barabarani)
Matumizi: Tutazikodisha tutapata kodi, na baadhi tutaendesha sisi wenyewe.
iv. MICHEZO:
Tutajenga michezo ya watoto, tutacheza sisi na tutakaribisha watoto toka nje ya CENTRE wakiingia watalipa kiingilio. Michezo kama bembea, kuogelea nk.
v. UENDESHAJI WA NURSERY NA VYUO VYA UFUNDI STADI:
Tutajenga maeneo ambayo tutaweka walimu na miundombinu ya kuwafundishia ufundi kama umeme, maji, useremala, ushonaji, magari nk. Pia tutaanza huduma ya Day care na Nursery school.
Matumizi: Tutafanikiwa kuwaingiza wale YATIMA wetu ambao wanaanza shule na wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari na hawana uwezo wa kuendelea. Tutakaribisha maombi kwa wanaotoka katika mashule mengine ili wajiunge na kulipa ada ili tupate pesa.
vi. KUMBI ZA MIKUTANO:
Tutajenga kumbi size mbalimbali kwa ajili ya matumizi hayo kwa jamii iliyotuzunguka. Matumizi: Tutazikodisha kwa bei nafuu ili tupate pesa ya kuendeleza familia hii.
vii. HOSTELS:
Tutajenga maeneo kwa ukubwa na quality mbalimbali kwa ajili ya wageni wataokuwa wakitembelea Yatima toka sehemu mbalimbali za dunia. Tutakodisha kwa kodi kidogo ili ugeni usiwe unasumbuka kwenda mbali na Centre. Tutajenga maeneo maalumu ya kufanyia ibada za MAFUNGO na TOBA katika hali ya utulivu mkubwa. Nazo wahitaji watalipa gharama kidodo. Hivyo ndani ya majengo tutaweka huduma za chakula na vinywaji kwa ajili ya wageni watakaokuwa wakiingia katika Centre mara kwa mara. NB: Maeneo ya ibada yatajengwa kulingana na mahitaji ya wana Centre lakini pia kwa kuzingatia UHITAJI wa wageni watakaoingia katika Centre. Eneo la kanisa na msikiti umetengwa na yatajengwa ili kila anayeingia katika Centre apate eneo la kujidai kwa kile anachotaka kukifanya katika imani yake.
viii. MAJUKUMU MAKUBWA YA MKURUGENZI MWANZILISHI.
Kwa kuwa janga la watoto kufiwa na wazazi na kutupwa hovyo limekuwa ni shida kubwa katika jamii katika Taifa letu na kwa kuwa tumeamua kushirikiana na Serikali katika kusaidia watoto Yatima na wale wanaotupwa. Taaisi yetu itabidi ijizatiti kweli kweli ili kupata FUND za kutosha kuhudumia familia ya Yatima ambayo tunaihudumia na ambayo iko mikononi mwetu. Hivyo atakuwa na majukumu makubwa kama ifuatavyo:-
a) Kutafuta wafadhili sehemu mbalimbali ili Taasisi iweze kupata fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa uendelezaji wa miradi yote itakayoanzishwa.
b) Kubuni miradi midogomidogo ya uzalishaji fedha.
c) Kukopa katika Taasisi za fedha mikopo isiyo na Riba au yenye riba kidogo na isiyo na masharti ya kuifilisi Taasisi.
d) Kuanzisha na kusimamia kwa karibu miradi yote ya taasisi ili kusudi kusiwepo uvujaji au upotevu wa kizembe.
e) Kuhakikisha kuwa watoto YATIMA wanapata elimu hadi ya chuo kikuu kulingana na uwezo wa kila mmoja kwa kushirikiana na Serikali.
f) Kutafuta (kununua/kuomba toka Serikalini) na kumiliki ardhi ya kutosha kwa ajili ya kupanua huduma za jamii ya MAYATIMA NJE YA KIBAHA.

F. MAISHA KATIKA MJI WA MUNGU VIKUGE.

Hii ni familia kama zilivyo familia zingine zenye wazazi. Tunapokea vichanga, tunalea, tunakuza na tunasomesha. Endapo watoto hawa watapata bahati wakafanya vizuri katika masomo yao na wakapata ajira yeyote ya kuwawezesha kujitegemea kwetu ni fahari kubwa sana. Watatoka katika MJI WA MUNGU wataenda nje kujitegemea. Endapo hawakubahatika kupata ajira nje ya mji wao watarudi nyumbani watafanya kazi za nyumbani kwa kushirikiana na wazazi wao na wadogo zao. Nyumbani kwao ni hapa MJI WA MUNGU VIKUGE. Popote maisha yao yatakapoishia (yaani kifo) watarudishwa nyumbani kwa maziko.

SIFA ZA MTU KUWA MKURUGENZI WA MJI WA MUNGU:

a) Kwa kuwa uanzishwaji wa MJI WA MUNGU ni wa kifamilia zaidi, hivyo uteuzi wa kuungoza MJI huu utakuwa umejengwa kifamilia zaidi.
b) WAKATI WA UTEUZI WA WAKURUGENZI WASAIDIZI.
Mkurugenzi mkuu mwanzilishi nilikaa na familia yangu tukapanga namna ya kuanzisha huduma hii kwa kujinyima ili watoto wadogo wanaofiwa au kutupwa na wazazi wao, wapate kuhudumiwa na familia yetu.
Sababu kubwa ikiwa ni kuchota Baraka kifamilia sasa na hata vizazi vijavyo. Hivyo Mkurugenzi Mkuu mara zote atatokana na Watoto/ Wajukuu wa Mkurugenzi mwanzilishi.
Wakurugenzi wasaidizi wataweza kuteuliwa toka miongoni mwa wachungaji waandamizi.Pia wataweza kutoka miongoni mwa wanafamilia toka MJI WA MUNGU ambao wamepokelewa kulelewa na kusomeshwa na Taasisi ya MJI WA MUNGU VIKUGE.

MWISHO.

Ninamshukuru MUNGU kunipa nafasi na uwezo wa kufanya kazi hii ambayo ninaamini ni njema machoni pake. Ninamwomba MUNGU alinde MJI huu wake nilioujenga kwa uwezo wake ili uwe Baraka kwa familia yangu na kwa waamini wote wanaoamini uwepo wa MUNGU katika maisha ya wanadamu na viumbe wote.
TUMSIFU YESU KRISTO.

Imetayarishwa na kuletwa kwenu na

Rabbo Joachim M. Thobias
(Mkurugenzi Mkuu Mwanzilishi)

Follow Us On

Facebook

Instagram

Tiktok

Twitter

Contacts

Postal Adress
P.O.Box 13070 Kibamba, Daresalaam,Tanzania
Email: emischoolscentre2020@gmail.com
Website: www.emischoolscentre.co
Director: 0712557324
Headteacher Primary: 0628994514
Headteacher Secondary: 0765864686
Academic Primary: 0713727915

Location